Monday, December 24, 2012

Wakati huu wa Sikukuu, Jeshi la Polisi Tanzania linakumbusha yafuatayo...

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA

Anuani ya Simu “MKUUPOLISI” 
Ofisi ya  Inspekta  Jenerali wa Polisi, 
Simu : (022) 2110734 
Fax Na. (022) 2135556
Unapojibu tafadhali taja: 
                               Makao Makuu ya Polisi,
 S.L.P. 9141,
DAR ES SALAAM.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

DAR ES SALAAM DISEMBA 24, 2012.

1. Jeshi la Polisi Nchini, linawakumbusha wananchi wote kuwa, tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya itakayoadhimishwa kati ya tarehe 24-26 Disemba, 2012 na tarehe 01 Januari, 2013 wanatakiwa kusherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa sheria. Wananchi wote wachukue tahadhali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya uhalifu na wahalifu kwenye maeneo mbalimbali vinadhibitiwa.

2. Ikumbukwe kuwa, wananchi wenye imani ya Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe, uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho cha sikukuu kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu.

3. Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba wananchi kote nchini wanasherekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

4. Aidha, tunawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani, madereva kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.

5. Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. Vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto na kutokuwaacha kutembea peke yao, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu ya watoto hao.

6. Wananchi wote wanakumbushwa kwamba, watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na endapo kuna ulazima wa kufanya hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka kwa wahusika kupitia namba simu 0754 785557 ama namba za viongozi wa polisi zilizokwishatolewa hapo awali.

7. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali, madhehebu ya dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa, vyombo vya habari, makampuni binafsi ya ulinzi na wananchi kwa ujumla, kuendelea kutoa ushirikiano na hasa katika kipindi cha mwisho wa mwaka, ili kuhakikisha usalama wa nchi yetu unadumishwa na raia wote wema wanaishi kwa amani na utulivu bila hofu ya uhalifu.

8. Mwisho, nawahakikishia wananchi kwamba, Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria za nchi na hivyo halitawajibika kumwonea huruma ama upendeleo mtu yeyote atakayeenda kinyume na sheria.

NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE KHERI YA CHRISTMAS NA MWAKA MPYA.

Imetolewa na:
Advera Senso-ASP
Msemaji wa Jeshi la Polisi (T)
POLISI MAKAO MAKUU.

No comments: