Saturday, March 2, 2013

Majina ya Tume ya Waziri Mkuu ya kuchunguza Matokeo CSEE 2012

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo Jumamosi, Machi 2, 2013 amezindua Tume maalum aliyoiunda ili ifanye uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo watafute kiini cha mserereko wa kushuka kwa ufaulu kuanzia mwaka 2010 hadi 2012.

Waziri Mkuu amezungumza na wajumbe wa Tume hiyo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk  Shukuru Kawambwa.

Amesema kwa  mujibu wa hadidu za rejea, wajumbe wa tume hiyo watatakiwa kuangalia ni sababu zipi zimechangia kuwepo kwa matokeo hayo mabaya, mserereko wa kushuka umekuwa ukiongezeka kwa sababu gani, usimamizi katika Halmashauri ukoje, ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya elimu kwenye Wizara ya TAMISEMi umechangiaje kushuka kwa kiwango cha ufaulu.

Vilevile, watatakiwa kuangalia mitaala na mihutasari ikoje, kuangalia uwiano uliopo kwenye mitihani inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani hiyo; kuangalia mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji, usimamizi na uendeshaji, na kutokuwepo kwa chakula shuleni kunachangiaje kushuka kwa utendaji mbaya wa wanafunzi katika masomo yao.

Tume hiyo yenye wajumbe 15, imepewa muda wa wiki sita kuanzia Machi mosi iwe imekamilisha kazi hiyo na kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu.

Tume itaongozwa na Prof. Sifuni Mchome wa Tume ya Vyuo Vikuu, na Makamu wake atakuwa Bi. Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti Maalum – Kagera).

Wajumbe wengine ni Bw. James Mbatia (mbunge wa Kuteuliwa), Bw. Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti), Prof. Mwajabu Possi (Chuo Kikuu - UDSM), Bibi Honoratha Chitanda (CWT), Bibi Daina Matemu (TAHOSSA) na Bw. Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).

No comments: