Thursday, March 21, 2013

RC ISSA MACHIBYA: DHIBITINI UHALIFU KUPITIA MITANDAO YA SIMU


Mkuu wa mkoa kigoma Issa Machibya amezitaka kampuni za simu za mkononi kuweka udhibiti wa kutosha kwa mitandao yao ya simu ili kuzuia vitendo vya utapeli na uhalifu ambavyo vimechangiwa na simu hizo.

Akifungua kikao cha siku moja cha wadau wa mawasiliano jana kilichoitishwa na mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) Machibya alisema kuwa mitandao ya simu imekuwa ikitumika sana kwa sasa katika kufanyia utapeli lakini juhudi za kuwakamata wahusika hazizai matunda. 

Alisema kuwa moja ya sababu za kushindwa kukamatwa kwa wahalifu hao ni pamoja na kusajili kwa kutumia majina bandia jambo ambalo amesema linaviwia vigumu vyombo vya usalama kuwamakata wahusika waliojiandikisha kwa majina bandia. 

Ili kufanikisha kuhakikisha mwenye simu ndiye mwenye jina halisi amezitaka kampuni za simu kuhakikisha kwamba mawakala wao wanaouuza laini za simu wanapata vitambulisho sahihi vya wahusika na kutokubali kusajili namba ya simu kama mhusika hana kitambulisho. 

Akizungumzia kuhusu kuanza kwa matumizi ya teknolojia ya digitali kutoka analojia Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wananchi wanapaswa kukubaliana na mabadiliko ya teknolojia kwani jambo hilo si la Tanzania peke yake bali ni suala la kidunia. 

Alisema kuwa jambo kubwa ambalo linapaswa kufanywa kwa sasa ni kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mfumo huo na kuona namna gani serikali na wadau mbalimbali wanashirikiana kuhakikisha wananchi wanatumia teknolojia hiyo kwa gharama nafuu. 

Kwa upande wake Meneja mipango na utafiti wa mamlaka ya mwasiliano nchini (TCRA), Ally Simba alisema kuwa moja ya kazi za mamlaka ni kuhakikisha teknolojia mbalimbali zilizo chini ya mamlaka hizo zinatumika bila kuleta athari kwa jamii na kwamba kutokana na hilo wanatarajia kukaa tena na wadau mbalimbali katika kuangalia suala la udhibiti wa simu za mkononi zisitumike vibaya. 

Asante kwa blog ya Mjengwa

No comments: