Sunday, November 11, 2012

Ni vita CCM Dodoma

VITA ya maneno ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inazidi kupamba moto, baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu taifa, Hussein Bashe kumtuhumu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akisema ndiye anakivuruga chama hicho. 

Mapambano hayo yanatokea wakati wanaCCM wanakutana mjini Dodoma kwa siku tatu katika mkutano wake mkuu, ambao utachagua viongozi wa kitaifa watakaokiongoza chama hicho pamoja na wajumbe wa Nec 10 kutoka Tanzania Bara na wengine kumi kutoka Zanzibar.

Bashe pia alimtuhumu Membe kuwa anawatumia vijana wawili ndani ya chama hicho kusambaza vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete na kumsingizia yeye na wenzake. 

Kauli ya Bashe inakuja siku moja baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho kutoka Mkoa wa Morogoro, Augustino Matefu kumtaja Bashe, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Beno Malisa na kada wa chama hicho, Fredrick Lowassa, kuwa wanahusika kutawanya vipeperushi hivyo. 

Vipeperushi hivyo, ambavyo vilitawanywa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma vilikuwa na ujumbe unaosomeka: “CCM inayumba, kwa pamoja tumpunguzie mzigo mheshimiwa Rais kwa kumvua kofia moja ya uenyekiti, nina imani kwa pamoja tutashinda, piga kura ya hapana kwake, CCM oyeeee.” 

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Bashe alikanusha taarifa hizo akisema kuwa hajawahi kufikiria kumpinga Rais Kikwete na kwamba maneno hayo ni uzushi juu yake. 
“Lazima niwaambie kuwa hayo ni makundi yanayotengenezwa na baadhi ya watu, ili kunichafulia jina langu. Mwaka jana nilisema kuwa nitakuja kumtaja mtu huyo na leo namtaja kuwa ni Benard Membe, ndiye anayenisakama kupitia vijana wake,” alisema Bashe.


Alisema kuwa Membe kupitia kwa vijana wawili aliowataja kuwa ni Makonda na Matefu, alianza kumsakama tangu Aprili mwaka uliopita baada ya yeye (Bashe), kuteuliwa na UVCCM kuongoza kamati ya kutafuta maoni ya kuihuisha jumuiya hiyo. 
“Kwanza lazima Watanzania wafahamu kuwa, Membe ni mwongo, asiyekuwa na msimamo wakati wote. Nilisema na leo nataka ujumbe umfikie na tayari nimeandika barua kwa Katibu Mkuu wa CCM kumjulisha hilo,” alisema Bashe. 

Pia alimtuhumu waziri huyo kuwa amekuwa akiishi kwa kubebwa wakati wote akitoa mfano kuwa, mwaka 2005 alibebwa na Rostam Aziz kwa kumpatia gari lililomwezesha kwenda kuomba kura za ubunge na akapata. 

Bashe pia alimtuhumu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwa ni mshirika wa Membe katika harakati hizo za kukichafua Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Nyalandu 
Hata hivyo, Nyalandu alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo jana, alisema: “Waongo sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto kwa kibiriti.” 

Membe 
 Alhamisi wiki hii, Membe alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa kuna kundi la watu ndani ya chama hicho, linalofanya kampeni chafu dhidi yake, lakini akasema kwamba hujuma hiyo haitafanikiwa, badala yake atashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Nec. ''Nakubaliana kabisa kwamba ziko njama za kunihujumu, ambazo hata mimi nazijua. Lakini wabaya wangu hao, wanafanya jambo ambalo hawalijui, kama wangejua wasingepoteza muda huo,'' alisema Membe.

Alijifananisha na mwembe, ambao hutupiwa mawe wakati wote kuliko mchongoma wenye miiba aliosema hauwezi kutupiwa mawe kwani hauna kitu cha kuchukua juu yake.

Wazee wanena
 
Baraza la Wazee wa CCM, Wilaya ya Dodoma Mjini jana walipinga kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kutaka madaraka ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa yatenganishwe. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Balozi Job Lusinde, alisema kuwa siyo jambo la busara hata kidogo kutenganisha nafasi hizo. Lusinde alisema kwamba ni vyema Rais akaachwa kuendelea na shughuli zake pamoja na kofia zote mbili kwa kuwa ndiyo msingi na kanuni za chama. 

Nec Vijana 
Kwa upande wao wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia kundi la vijana, walisema kuwa watamlinda kwa gharama yoyote Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete pamoja na kuhakikisha kuwa anapata kura zote za ‘ndiyo.’

Mbali na hilo, vijana hao walisema kuwa watafanya kila njia kumsaka mtu aliyetengeneza vipeperushi hivyo vinavyosambazwa dhidi ya mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete. Wajumbe hao saba kati ya kumi waliitisha mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma na kutoa tamko hilo, huku wakieleza kuwa hawatalala hadi watakapoona mwenyekiti wao akiibuka na ushindi wa kishindo. 

“Sisi ndiyo jeshi la chama. Itakuwa ni aibu kama mwenyekiti wetu atakuwa akidhalilishwa kwa kupata kura chache, ilhali nasi tupo. Lazima kuwaaibisha watu wa aina hiyo na kuwasaka popote walipo. Tunaomba vijana wenzetu watuamini kuwa tuko Dodoma kufanya kazi hiyo,” alisema Jery Silaa kwa niaba ya wenzake. 

CCM Kagera 
Naye Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kagera, Hamimu Omary, amekanusha uvumi uliozagaa kuwa Mkoa wa Kagera ni mmoja ya mikoa inayounga mkono mkakati wa kumhujumu Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete. 

www.mwananchi.co.tz

No comments: