Sunday, December 23, 2012

WAWILI WAUAWA KWA WIZI WA MBUZI

WATU wawili wakazi wa kijiji Nyamtukuza wilaya ya kibondo mkoani Kigoma wameuawa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali wakituhumiwa kuiba mbuzi wawili wenye thamani ya shilingi 40,000.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraiser Kashai aliwataja watu hao waliouawa kuwa ni Nongo Bufinkri (36) na Azimio Muhabwa ambao waliiba mbuzi mali ya Sibalina John na waliuawa juzi majira ya mchana kijiji hapo. 

Hata hivyo Kamanda Kashai alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambapo mtuhumiwa mmoja alifanikiwa kukimbia kabla ya wenzake kukutwa na mauti. 

Katika tukio lingine kamanda huyo wa polisi mkoa kigoma alisema kuwa mkulima mmoja mkazi wa kijiji cha Kazuramimba Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Stephano Muhunzi (70) aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni mjambazi.

Alisema kuwa katika tukio hilo watu watano walivamiwa nyumbani kwa marehemu majira ya mchana na baada ya kumjeruhi vibaya mwilini waliondoka na kondoo sita wenye thamani ya shilingi 300,000. 

Aidha hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye amekamatwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo na kwamba juhudi za kuwatafuta wauaji zinaendelea. 

Katika hatua nyingine Kamanda wa polisi mkoa kigoma, Fraiser Kashai amewataka wananchi mkoani Kigoma kujihadhari na watu wasiowema amabo wanafika kwenye makazi yao na kuwataka kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapohisi kuna kitu cha namna hiyo. 

Pia kamanda huyo wa polisi mkoa kigoma amesema kuwa jeshi lake limejipanga vizuri kuhakikisha kwamba kuna na amani na usalama wakati wote wa kipindi cha sikukuu za Christmas na mwaka mpya. 

Asante kwa KPC

No comments: