Wednesday, January 23, 2013

Lowassa aibua hukumu ya kifo

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amependekeza katiba mpya izuie adhabu ya kifo kwa kosa la kukusudia au uhaini hapa nchini na iruhusu elimu kutolewa bila malipo kwa shule za sekondari. Pia amependekeza katiba mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha fedha ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni za chaguzi za kuwania uongozi na pia ifafanue rushwa ni nini kwenye chaguzi hizo. Mapendekezo hayo, ambayo ni sehemu ya maoni ya Lowassa kuhusu uundwaji wa katiba mpya, aliyatoa alipokutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam jana. 

ADHABU YA KIFO 
Lowassa alisema katiba ya sasa haisemi wazi kuhusu adhabu ya kifo, badala yake inazungumzia tu haki ya uhai. Alisema Ibara ya 14 ya katiba ya sasa inatamka kijumla tu kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na uhai wake kulindwa, lakini haki hiyo inanyang’anywa na kifungu namba 196 cha sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16, kinachotamka kuwa adhabu ya kifo kwa kosa la mauaji ya kukusudia na kwamba adhabu hiyo hiyo pia hutolewa kwa kosa la uhaini. “Sasa mapendekezo yangu mimi ni kwamba, kuwe na ibara katika katiba mpya inayotamka wazi kuwa hakutakuwa na adhabu ya kifo hapa nchini hata kwa kosa la kukusudia au uhaini,” alisema Lowassa. 

ELIMU BURE 
Kuhusu elimu bila malipo, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM) alisema moja ya haki za mtoto ni kupata elimu hivyo, alipendekeza suala la elimu bure ya sekondari liwekwe kwenye katiba ya nchi. “Katiba itamke wazi kuwa elimu ya sekondari ni bure,” alisema Lowassa na kuongeza: “Nchi bado ina idadi kubwa ya watu maskini, ambao uwezo wao wa kipato ni mdogo.” Kutokana na hali hiyo, alisema anaamini suala hilo linawezekana na serikali inaweza kugharimia elimu ya sekondari ili iwe bure kwa wote. Alisema mfumo huo utatoa nafasi ya kujenga taifa lijalo lenye idadi kubwa ya vijana watakaokuwa wamepata elimu ya sekondari. “Wabunge wenzangu bila shaka wanalijua hili. Ukweli katika majimbo yetu wazazi wamekuwa wakishindwa kulipia karo ya shule kwa watoto wao. Wabunge tumekuwa tukibeba mzigo huo japo kidogo. Kwa hiyo, kifungu cha elimu bure kwa sekondari, kiwapo kwenye katiba,” alisema Lowassa. Pendekezo la kutaka elimu ya bure linafanana na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) ya mwaka 2010 ambayo kiliahidi kuwa kingetoa elimu ya bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari. Ilani hiyo ilisema: “Elimu ya ngazi ya msingi na sekondari itagharimiwa na serikali kuu pamoja na serikali za mitaa. Lengo ni kuhakikisha kuwa elimu hii ya msingi kabisa itakuwa ni haki kwa kila mtoto wa Kitanzania na kiwango cha ubora kinalingana kwa nchi nzima.”

MATUMIZI YA FEDHA KATIKA UCHAGUZI
 Lowassa alisema katika sehemu nyingi nchini, mwananchi kama hana fedha hawezi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Hivyo, alipendekeza katiba mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha fedha, ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni. Pia alipendekeza ibara hiyo iainishe ni matumizi gani ya lazima, ambayo mgombea hawezi kukwepa kutumia fedha katika kampeni zake. “Mfano, kuwakusanya wapigakura kwenda kupiga kura gharama hizo nani azibebe,” alisema Lowassa. Pia alipendekeza Katiba Mpya ifafanue rushwa ni nini kwenye chaguzi hizo. “Au tuwe na proportional representation (uwakilishi wa uwiano), vyama viwe ndiyo vinaingia kwenye chaguzi kuwania majimbo na siyo wanachama, huko kila mtu atakuwa anapigania chama chake kupata kura nyingi ili wapate viti vingi zaidi, pengine hii itasaidia kuondoa kikwazo cha mtu kuwa na uwezo wa kifedha ndiyo aweze kuwania uongozi,” alisema Lowassa. 

ARDHI 
Lowassa alisema kwa mwanadamu, kunyang’anywa haki ya kutumia ardhi ya nchi aliyozaliwa ni sawa na kunyang’anywa haki ya uraia wake. Alisema katiba ya sasa inawapa nguvu wakulima katika suala la ardhi na kuwasahau wafugaji, ambao alisema wamekuwa wakimbizi katika nchi yao. “Wamekuwa wakitangatanga kutafuta malisho ya mifugo yao. Ile ardhi waliyokuwa wanaimiliki wakiondoka kutafuta malisho huku nyuma imekuwa ikimilikishwa watu wengine; wakulima au wawekezaji. Hili kwakweli si jambo jema. Tumeshuhudia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji,” alisema. Kutokana na hali hiyo, alipendekeza katiba mpya impe mfugaji haki katika suala la ardhi kama wakulima na ardhi ya wafugaji ilindwe, ikiwa ni pamoja na haki hiyo kufafanuliwa kikatiba. Pia alipendekeza kuwapo na hali ya usawa (50,50 situation) kati ya mfugaji na mkulima katika suala zima la umiliki wa ardhi kikatiba. 
CHANZO: NIPASHE

No comments: